سورة الحشر

Surat Al-Hashr kwa Kiswahili

Uhamisho

Msahafu

Mishary Rashid AlafasyPakua MP3Pakua PDF

Surat Al-Hashr (الحشر) ni sura ya 59 katika Qur’ani na ina aya 24. Jina lake lina maana ya “Uhamisho”. Ni sura ya Madina, iliyoteremshwa Madina baada ya Hijra, na iko katika juzuu ya 28.

Katika ukurasa huu unaweza kusoma Surat Al-Hashr yote kwa Kiarabu, pamoja na tafsiri ya Kiswahili ya Ali Muhsin Al-Barwani aya kwa aya na matamshi kwa herufi za Kilatini, na kusikiliza kisomo chake.

Surat Al-Hashr kamili: Kiarabu, tafsiri ya Kiswahili na matamshi

بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَـٰنِ ٱلرَّحِيمِ

  1. سَبَّحَ لِلَّهِ مَا فِى ٱلسَّمَـٰوَٰتِ وَمَا فِى ٱلْأَرْضِ ۖ وَهُوَ ٱلْعَزِيزُ ٱلْحَكِيمُ۝١

    Sabbaha lillahi ma fee alssamawati wama fee alardi wahuwa alʿazeezu alhakeemu

    Vinamsabihi, Vinamtakasa Mwenyezi Mungu viliomo katika mbingu na viliomo katika ardhi. Naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.1

    Maelezo
    [1] Vitu vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi vinamtakasa Mwenyezi Mungu na kila lisio laiki naye. Na Yeye ndiye Mwenye kushinda ambaye hashindwi na kitu. Mwenye hikima katika mipango yake na vitendo vyake.
  2. هُوَ ٱلَّذِىٓ أَخْرَجَ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ مِنْ أَهْلِ ٱلْكِتَـٰبِ مِن دِيَـٰرِهِمْ لِأَوَّلِ ٱلْحَشْرِ ۚ مَا ظَنَنتُمْ أَن يَخْرُجُوا۟ ۖ وَظَنُّوٓا۟ أَنَّهُم مَّانِعَتُهُمْ حُصُونُهُم مِّنَ ٱللَّهِ فَأَتَىٰهُمُ ٱللَّهُ مِنْ حَيْثُ لَمْ يَحْتَسِبُوا۟ ۖ وَقَذَفَ فِى قُلُوبِهِمُ ٱلرُّعْبَ ۚ يُخْرِبُونَ بُيُوتَهُم بِأَيْدِيهِمْ وَأَيْدِى ٱلْمُؤْمِنِينَ فَٱعْتَبِرُوا۟ يَـٰٓأُو۟لِى ٱلْأَبْصَـٰرِ۝٢

    Huwa allathee akhraja allatheena kafaroo min ahli alkitabi min diyarihim liawwali alhashri ma thanantum an yakhrujoo wathannoo annahum maniʿatuhum husoonuhum mina Allahi faatahumu Allahu min haythu lam yahtasiboo waqathafa fee quloobihimu alrruʿba yukhriboona buyootahum biaydeehim waaydee almumineena faiʿtabiroo ya olee alabsari

    Yeye ndiye aliye watoa walio kufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu katika nyumba zao wakati wa uhamisho wa kwanza. Hamkudhani kuwa watatoka, nao walidhani kuwa ngome zao zitawalinda na Mwenyezi Mungu. Lakini Mwenyezi Mungu aliwafikia kwa mahali wasipo patazamia, na akatia woga katika nyoyo zao. Wakawa wanazibomoa nyumba zao kwa mikono yao na mikono ya Waumini. Basi zingatieni enyi wenye macho!2

    Maelezo
    [2] Yeye Mwenyezi Mungu ndiye aliye watoa walio kufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu, nao ni Mayahudi wa ukoo wa Banu Nnadhir, kutoka kwenye majumba yao wakati wa kuwatoa mara ya kwanza katika Bara Arabu. Enyi Waislamu! Hamkudhania kuwa watatoka kwenye nyumba zao kwa sababu ya nguvu zao. Na wao wenyewe walidhani kwamba ngome zao zitawalinda na mashambulio ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu akawatokea katika upande wasio utarajia, na akawatia katika nyoyo zao fazaa kubwa, wakawa wanabomoa nyumba zao kwa mikono yao ili zibaki kuwa magofu tu, na kwa mikono ya Waumini wapate kuzivunja zile ngome. Basi enyi wenye akili, chukueni somo katika haya yaliyo washukia hawa.
  3. وَلَوْلَآ أَن كَتَبَ ٱللَّهُ عَلَيْهِمُ ٱلْجَلَآءَ لَعَذَّبَهُمْ فِى ٱلدُّنْيَا ۖ وَلَهُمْ فِى ٱلْـَٔاخِرَةِ عَذَابُ ٱلنَّارِ۝٣

    Walawla an kataba Allahu ʿalayhimu aljalaa laʿaththabahum fee alddunya walahum fee alakhirati ʿathabu alnnari

    Na lau kuwa Mwenyezi Mungu asingeli waandikia kutoka, angeli waadhibu katika dunia. Na katika Akhera watapata adhabu ya Moto.3

    Maelezo
    [3] Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hakuwahukumia kuwatoa majumbani kwao kwa sura hii ya kuchusha, basi hapana shaka angeli waadhibu katika dunia kwa shida zaidi kuliko huko kuwatoa. Na Akhera, wao watapata adhabu ya Moto, mbali huku kutolewa majumbani kwao duniani.
  4. ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ شَآقُّوا۟ ٱللَّهَ وَرَسُولَهُۥ ۖ وَمَن يُشَآقِّ ٱللَّهَ فَإِنَّ ٱللَّهَ شَدِيدُ ٱلْعِقَابِ۝٤

    Thalika biannahum shaqqoo Allaha warasoolahu waman yushaqqi Allaha fainna Allaha shadeedu alʿiqabi

    Hayo ni kwa sababu walimpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mwenye kumpinga Mwenyezi Mungu, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.4

    Maelezo
    [4] Hayo yaliyo wapata duniani na yanayo wangojea Akhera ni kwa sabau ya kuwa wamemfanyia uadui Mwenyezi Mungu na Mtume wake, uadui mkubwa mno. Na mwenye kumfanyia uadui Mwenyezi Mungu basi hawezi kupenya kuikimbia adhabu yake. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
  5. مَا قَطَعْتُم مِّن لِّينَةٍ أَوْ تَرَكْتُمُوهَا قَآئِمَةً عَلَىٰٓ أُصُولِهَا فَبِإِذْنِ ٱللَّهِ وَلِيُخْزِىَ ٱلْفَـٰسِقِينَ۝٥

    Ma qataʿtum min leenatin aw taraktumooha qaimatan ʿala osooliha fabiithni Allahi waliyukhziya alfasiqeena

    Mtende wowote mlio ukata au mlio uacha unasimama vile vile juu ya mashina yake, basi ni kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na kwa kuwahizi wapotovu.5

    Maelezo
    [5] Enyi Waislamu! Mitende yoyote mliyo ikata au mkaiacha imebaki kama ilivyo kuwa, basi ni kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Hapana lawama juu yenu katika hayo, ili awape nguvu Waumini, na awahizi wapotovu walio ziacha sharia zake.
  6. وَمَآ أَفَآءَ ٱللَّهُ عَلَىٰ رَسُولِهِۦ مِنْهُمْ فَمَآ أَوْجَفْتُمْ عَلَيْهِ مِنْ خَيْلٍ وَلَا رِكَابٍ وَلَـٰكِنَّ ٱللَّهَ يُسَلِّطُ رُسُلَهُۥ عَلَىٰ مَن يَشَآءُ ۚ وَٱللَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَىْءٍ قَدِيرٌ۝٦

    Wama afaa Allahu ʿala rasoolihi minhum fama awjaftum ʿalayhi min khaylin wala rikabin walakinna Allaha yusallitu rusulahu ʿala man yashao waAllahu ʿala kulli shayin qadeerun

    Na mali aliyo leta Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kutoka kwao hamkuyakimbilia mbio kwa farasi wala ngamia. Lakini Mwenyezi Mungu huwapa mamlaka Mitume wake juu ya wowote awatakao. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.6

    Maelezo
    [6] Na aliyo yaleta Mwenyezi Mungu na akayarudisha kwa Mtume wake katika mali ya Banu Nnadhir hamkuyapigia mbio nyinyi kwa farasi wala ngamia. Lakini Mwenyezi Mungu huwapa madaraka Mitume wake kwa awatakao katika waja wake bila ya kupigana vita. Na Mwenyezi Mungu ni Mtimilivu wa uweza juu ya kila kitu.
  7. مَّآ أَفَآءَ ٱللَّهُ عَلَىٰ رَسُولِهِۦ مِنْ أَهْلِ ٱلْقُرَىٰ فَلِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ وَلِذِى ٱلْقُرْبَىٰ وَٱلْيَتَـٰمَىٰ وَٱلْمَسَـٰكِينِ وَٱبْنِ ٱلسَّبِيلِ كَىْ لَا يَكُونَ دُولَةًۢ بَيْنَ ٱلْأَغْنِيَآءِ مِنكُمْ ۚ وَمَآ ءَاتَىٰكُمُ ٱلرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَىٰكُمْ عَنْهُ فَٱنتَهُوا۟ ۚ وَٱتَّقُوا۟ ٱللَّهَ ۖ إِنَّ ٱللَّهَ شَدِيدُ ٱلْعِقَابِ۝٧

    Ma afaa Allahu ʿala rasoolihi min ahli alqura falillahi walilrrasooli walithee alqurba waalyatama waalmasakeeni waibni alssabeeli kay la yakoona doolatan bayna alaghniyai minkum wama atakumu alrrasoolu fakhuthoohu wama nahakum ʿanhu faintahoo waittaqoo Allaha inna Allaha shadeedu alʿiqabi

    Mali aliyo leta Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kutoka kwa watu wa hivi vijiji ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na kwa ajili ya Mtume, na jamaa, na mayatima, na masikini, na msafiri, ili yasiwe yakizunguka baina ya matajiri tu miongoni mwenu. Na anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.7

    Maelezo
    [7] Alicho rudisha Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake katika mali ya watu wa vijiji hivi bila ya kuwatimua farasi au ngamia, vitu hivyo ni vya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na jamaa, na mayatima, na masikini, na wasafiri. Haya ni hivyo ili yasiwe mali yakizunguka katika mikono ya matajiri peke yao katika nyinyi. Na anacho kupeni Mtume katika hukumu basi kishikeni, na anacho kukatazeni basi kiwacheni. Na jilindeni na kughadhibika kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
  8. لِلْفُقَرَآءِ ٱلْمُهَـٰجِرِينَ ٱلَّذِينَ أُخْرِجُوا۟ مِن دِيَـٰرِهِمْ وَأَمْوَٰلِهِمْ يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ ٱللَّهِ وَرِضْوَٰنًا وَيَنصُرُونَ ٱللَّهَ وَرَسُولَهُۥٓ ۚ أُو۟لَـٰٓئِكَ هُمُ ٱلصَّـٰدِقُونَ۝٨

    Lilfuqarai almuhajireena allatheena okhrijoo min diyarihim waamwalihim yabtaghoona fadlan mina Allahi waridwanan wayansuroona Allaha warasoolahu olaika humu alssadiqoona

    Wapewe mafakiri Wahajiri walio tolewa majumbani mwao na mali yao kwa ajili ya kutafuta fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi zake, na wanamsaidia Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao ndio wa kweli.8

    Maelezo
    [8] Na hivyo yale mali ya watu wa vijiji aliyo yarudisha Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake wapewe mafakiri katika Wahajiri, walio kimbilia Madina, ambao wametolewa majumbani kwao na mali yao huko Makka. Wao wanataraji ziada kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika riziki zao na radhi. Na wanamsaidia Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa nafsi zao na mali yao. Hao ndio Waumini wa kweli.
  9. وَٱلَّذِينَ تَبَوَّءُو ٱلدَّارَ وَٱلْإِيمَـٰنَ مِن قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ وَلَا يَجِدُونَ فِى صُدُورِهِمْ حَاجَةً مِّمَّآ أُوتُوا۟ وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰٓ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِۦ فَأُو۟لَـٰٓئِكَ هُمُ ٱلْمُفْلِحُونَ۝٩

    Waallatheena tabawwaoo alddara waaleemana min qablihim yuhibboona man hajara ilayhim wala yajidoona fee sudoorihim hajatan mimma ootoo wayuthiroona ʿala anfusihim walaw kana bihim khasasatun waman yooqa shuhha nafsihi faolaika humu almuflihoona

    Na walio na maskani zao na Imani yao kabla yao, wanawapenda walio hamia kwao, wala hawaoni choyo katika vifua vyao kwa walivyo pewa (Wahajiri), bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji. Na mwenye kuepushwa uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufanikiwa.9

    Maelezo
    [9] Na Ma-ansari, watu wa Madina walio mnusuru Mtume na Wahajiri, ambao wamekaa Madina katika maskani zao, na Imani yao ikawa safi kabisa kabla ya kufika Wahajiri, wanawapenda wale wageni Waislamu walio hamia kwao, na wala hawahisi ubaya wowote katika nafsi zao kwa walicho pewa Wahajiri katika ngawira. Bali wanawakadimisha Wahajiri kuliko nafsi zao, ijapo kuwa wakiwa wao nao ni wahitaji. Na mwenye kuhifadhika, kwa uweza wa Mwenyezi Mungu, asione ubakhili katika nafsi yake, basi watu kama hao ndio wenye kufuzu kwa kila walipendalo.
  10. وَٱلَّذِينَ جَآءُو مِنۢ بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا ٱغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَٰنِنَا ٱلَّذِينَ سَبَقُونَا بِٱلْإِيمَـٰنِ وَلَا تَجْعَلْ فِى قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ رَبَّنَآ إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ۝١٠

    Waallatheena jaoo min baʿdihim yaqooloona rabbana ighfir lana waliikhwanina allatheena sabaqoona bialeemani wala tajʿal fee quloobina ghillan lillatheena amanoo rabbana innaka raoofun raheemun

    Na walio kuja baada yao wanasema: Mola wetu Mlezi! Tughufirie sisi na ndugu zetu walio tutangulia kwa Imani, wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani kwa walio amini. Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe ni Mpole na Mwenye kurehemu.10

    Maelezo
    [10] Na Waumini walio kuja baada ya Wahajiri na Ansari husema: Mola wetu Mlezi! Tusamehe dhambi zetu, sisi na ndugu zetu walio tutangulia katika Imani. Wala usijaalie kuwa katika nyoyo zetu husda kuwahusudu walio amini. Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe umefika ukomo katika upole na kurehemu.
  11. ۞ أَلَمْ تَرَ إِلَى ٱلَّذِينَ نَافَقُوا۟ يَقُولُونَ لِإِخْوَٰنِهِمُ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ مِنْ أَهْلِ ٱلْكِتَـٰبِ لَئِنْ أُخْرِجْتُمْ لَنَخْرُجَنَّ مَعَكُمْ وَلَا نُطِيعُ فِيكُمْ أَحَدًا أَبَدًا وَإِن قُوتِلْتُمْ لَنَنصُرَنَّكُمْ وَٱللَّهُ يَشْهَدُ إِنَّهُمْ لَكَـٰذِبُونَ۝١١

    Alam tara ila allatheena nafaqoo yaqooloona liikhwanihimu allatheena kafaroo min ahli alkitabi lain okhrijtum lanakhrujanna maʿakum wala nuteeʿu feekum ahadan abadan wain qootiltum lanansurannakum waAllahu yashhadu innahum lakathiboona

    Huwaoni wanao fanya unaafiki wanawaambia ndugu zao walio kufuru katika Watu wa Kitabu: Mkitolewa na sisi lazima tutatoka pamoja nanyi, wala hatutamt'ii yeyote kabisa dhidi yenu. Na mkipigwa vita lazima tutakusaidieni. Na Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa hao hakika bila ya shaka ni waongo.11

    Maelezo
    [11] Hebu huwaangalii hao wanaafiki ukastaajabu? Kazi yao ni kuwakariria kauli ndugu zao walio kufuru katika Watu wa Kitabu - nao ni hao Banu Nnadhir - kuwaambia: Wallahi! Mkilazimishwa kuihama Madina, basi hapana shaka na sisi tutatoka pamoja nanyi. Wala hatutamt'ii katika jambo lenu mtu yeyote daima dawamu. Na pindi ikiwa Waislamu watakupigeni vita, basi hapana shaka sisi tutakusaidieni. Na Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa hakika wanaafiki hapana shaka ni waongo katika hizo ahadi zao wanazo zitoa.
  12. لَئِنْ أُخْرِجُوا۟ لَا يَخْرُجُونَ مَعَهُمْ وَلَئِن قُوتِلُوا۟ لَا يَنصُرُونَهُمْ وَلَئِن نَّصَرُوهُمْ لَيُوَلُّنَّ ٱلْأَدْبَـٰرَ ثُمَّ لَا يُنصَرُونَ۝١٢

    Lain okhrijoo la yakhrujoona maʿahum walain qootiloo la yansuroonahum walain nasaroohum layuwallunna aladbara thumma la yunsaroona

    Pindi wakitolewa hawatatoka pamoja nao, na wakipigwa vita hawatawasaidia. Na kama wakiwasaidia basi watageuza migongo; kisha hawatanusuriwa.12

    Maelezo
    [12] Wakitolewa Mayahudi, wanaafiki hawatatoka pamoja nao. Na wakipigwa vita hawatawanusuru. Na pindi wakiwasaidia basi hapana shaka watatoka mbio warudi kinyume nyume, wala hawatawanusuru.
  13. لَأَنتُمْ أَشَدُّ رَهْبَةً فِى صُدُورِهِم مِّنَ ٱللَّهِ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَفْقَهُونَ۝١٣

    Laantum ashaddu rahbatan fee sudoorihim mina Allahi thalika biannahum qawmun la yafqahoona

    Hakika nyinyi ni kitisho zaidi katika vifua vyao kuliko Mwenyezi Mungu. Hayo ni kwa kuwa hao ni watu wasio fahamu kitu.13

    Maelezo
    [13] Hakika, enyi Waislamu, mna kitisho zaidi katika vifua vya wanaafiki na Mayahudi kuliko wanavyo mwogopa Mwenyezi Mungu. Hayo ni kwa sababu hakika wao ni watu wasio jua ukweli wa Imani.
  14. لَا يُقَـٰتِلُونَكُمْ جَمِيعًا إِلَّا فِى قُرًى مُّحَصَّنَةٍ أَوْ مِن وَرَآءِ جُدُرٍۭ ۚ بَأْسُهُم بَيْنَهُمْ شَدِيدٌ ۚ تَحْسَبُهُمْ جَمِيعًا وَقُلُوبُهُمْ شَتَّىٰ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَعْقِلُونَ۝١٤

    La yuqatiloonakum jameeʿan illa fee quran muhassanatin aw min warai judurin basuhum baynahum shadeedun tahsabuhum jameeʿan waquloobuhum shatta thalika biannahum qawmun la yaʿqiloona

    Hawatapigana nanyi kwa mkusanyiko isipo kuwa katika vijiji vilivyo zatitiwa kwa ngome, au nyuma ya kuta. Wao kwa wao vita vyao ni vikali. Utawadhania kuwa wako pamoja, kumbe nyoyo zao ni mbali mbali. Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasio na akili.14

    Maelezo
    [14] Mayahudi hawapigani vita nanyi kwa pamoja ila wawe katika miji iliyo jengewa ngome, au wajifiche nyuma ya kuta. Vita vyao baina ya wao kwa wao ni vikali. Utawadhani kuwa wameshikamana, wote ni wamoja. Kumbe hakika nyoyo zao zimefarikiana mbali mbali. Wao ni wenye sifa hizo, kwa sababu hao ni watu wasio zingatia nini utakuwa mwisho wa mambo.
  15. كَمَثَلِ ٱلَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ قَرِيبًا ۖ ذَاقُوا۟ وَبَالَ أَمْرِهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ۝١٥

    Kamathali allatheena min qablihim qareeban thaqoo wabala amrihim walahum ʿathabun aleemun

    Ni kama mfano wa walio kuwa kabla yao hivi karibuni. Walionja uovu wa mambo yao. Nao watapata adhabu iliyo chungu.15

    Maelezo
    [15] Mfano wa Bani Nnadhir ni kama mfano wa walio kufuru kabla yao karibuni. Hao walionja hapa hapa duniani matokeo ya ukafiri wao na kuvunja kwao mapatano. Na Akhera watapata adhabu ya uchungu mkali.
  16. كَمَثَلِ ٱلشَّيْطَـٰنِ إِذْ قَالَ لِلْإِنسَـٰنِ ٱكْفُرْ فَلَمَّا كَفَرَ قَالَ إِنِّى بَرِىٓءٌ مِّنكَ إِنِّىٓ أَخَافُ ٱللَّهَ رَبَّ ٱلْعَـٰلَمِينَ۝١٦

    Kamathali alshshaytani ith qala lilinsani okfur falamma kafara qala innee bareeon minka innee akhafu Allaha rabba alʿalameena

    Ni kama mfano wa Shetani anapo mwambia mtu: Kufuru. Na akikufuru humwambia: Mimi si pamoja nawe. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.16

    Maelezo
    [16] Mfano wa wanaafiki kuwashawishi Banu Nnadhir wamuasi Mtume wa Mwenyezi ni kama mfano wa Shetani pale anapo mghuri mtu aiache Imani, akamwambia: Kufuru! Na alipo kufuru akasema: Mimi niko mbali nawe, kwani mimi ninamkhofu Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.
  17. فَكَانَ عَـٰقِبَتَهُمَآ أَنَّهُمَا فِى ٱلنَّارِ خَـٰلِدَيْنِ فِيهَا ۚ وَذَٰلِكَ جَزَٰٓؤُا۟ ٱلظَّـٰلِمِينَ۝١٧

    Fakana ʿaqibatahuma annahuma fee alnnari khalidayni feeha wathalika jazao alththalimeena

    Basi ikawa mwisho wa wote wawili hao ni kuingia Motoni, wadumu humo daima; na hiyo ndiyo jaza ya madhaalimu.17

    Maelezo
    [17] Ikawa basi marejeo ya Shetani na huyo anaye mzaini ni kuishia Motoni wabaki humo milele. Na kudumu humo dawamu ni malipo ya wenye kuasi wakaikiuka Njia ya Haki.
  18. يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ ٱتَّقُوا۟ ٱللَّهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍ ۖ وَٱتَّقُوا۟ ٱللَّهَ ۚ إِنَّ ٱللَّهَ خَبِيرٌۢ بِمَا تَعْمَلُونَ۝١٨

    Ya ayyuha allatheena amanoo ittaqoo Allaha waltanthur nafsun ma qaddamat lighadin waittaqoo Allaha inna Allaha khabeerun bima taʿmaloona

    Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kila nafsi iangalie inayo yatanguliza kwa ajili ya Kesho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari ya mnayo yatenda.18

    Maelezo
    [18] Enyi mlio amini! Jiwekeeni kinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa kujilazimisha kumt'ii Yeye. Na kila nafsi izingatie a'mali gani ya kuikadimisha kwa ajili ya Kesho. Na jilazimisheni kumcha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari vilivyo kwa yote myatendayo. Naye atakulipeni kwa hayo.
  19. وَلَا تَكُونُوا۟ كَٱلَّذِينَ نَسُوا۟ ٱللَّهَ فَأَنسَىٰهُمْ أَنفُسَهُمْ ۚ أُو۟لَـٰٓئِكَ هُمُ ٱلْفَـٰسِقُونَ۝١٩

    Wala takoonoo kaallatheena nasoo Allaha faansahum anfusahum olaika humu alfasiqoona

    Wala msiwe kama wale walio msahau Mwenyezi Mungu, na Yeye akawasahaulisha nafsi zao. Hao ndio wapotovu.19

    Maelezo
    [19] Enyi Waumini! Msiwe kama wale walio sahau haki za Mwenyezi Mungu, na Yeye akawasahaulisha nafsi zao, kwa kuwajaribu kwa mitihani, na wakawa hawajui linalo wafaa na linalo wadhuru. Hao ndio walio toka wakaacha ut'iifu wa Mwenyezi Mungu.
  20. لَا يَسْتَوِىٓ أَصْحَـٰبُ ٱلنَّارِ وَأَصْحَـٰبُ ٱلْجَنَّةِ ۚ أَصْحَـٰبُ ٱلْجَنَّةِ هُمُ ٱلْفَآئِزُونَ۝٢٠

    La yastawee ashabu alnnari waashabu aljannati ashabu aljannati humu alfaizoona

    Hawawi sawa watu wa Motoni na watu wa Peponi. Watu wa Peponi ndio wenye kufuzu.20

    Maelezo
    [20] Hawawi sawa watu wa Motoni wanao teswa, na watu wa Peponi wanao neemeshwa. Watu wa Peponi peke yao ndio wenye kufuzu kwa kila walipendalo.
  21. لَوْ أَنزَلْنَا هَـٰذَا ٱلْقُرْءَانَ عَلَىٰ جَبَلٍ لَّرَأَيْتَهُۥ خَـٰشِعًا مُّتَصَدِّعًا مِّنْ خَشْيَةِ ٱللَّهِ ۚ وَتِلْكَ ٱلْأَمْثَـٰلُ نَضْرِبُهَا لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ۝٢١

    Law anzalna hatha alqurana ʿala jabalin laraaytahu khashiʿan mutasaddiʿan min khashyati Allahi watilka alamthalu nadribuha lilnnasi laʿallahum yatafakkaroona

    Lau kuwa tumeiteremsha hii Qur'ani juu ya mlima, basi bila ya shaka ungeli uona ukinyenyekea, ukipasuka kwa khofu ya Mwenyezi Mungu. Na hiyo mifano tunawapigia watu ili wafikiri.21

    Maelezo
    [21] Lau tungeli iteremsha hii Qur'ani juu ya mlima wenye nguvu basi ungeli uona huo mlima, juu ya nguvu zake, unanyenyekea na unapasuka kwa kumwogopa Mwenyezi Mungu. Na hiyo ni mifano tunawaelezea watu ili wapate kuzingatia matokeo ya mambo yao.
  22. هُوَ ٱللَّهُ ٱلَّذِى لَآ إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ عَـٰلِمُ ٱلْغَيْبِ وَٱلشَّهَـٰدَةِ ۖ هُوَ ٱلرَّحْمَـٰنُ ٱلرَّحِيمُ۝٢٢

    Huwa Allahu allathee la ilaha illa huwa ʿalimu alghaybi waalshshahadati huwa alrrahmanu alrraheemu

    Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye tu. Mwenye kuyajua yaliyo fichikana na yanayo onekana. Yeye ndiye Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.22

    Maelezo
    [22] Yeye Mwenyezi Mungu ambaye hapana wa kuabudiwa kikweli isipo kuwa Yeye peke yake, Mwenye kujua lilio pita na lilioko sasa. Yeye ndiye Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
  23. هُوَ ٱللَّهُ ٱلَّذِى لَآ إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ٱلْمَلِكُ ٱلْقُدُّوسُ ٱلسَّلَـٰمُ ٱلْمُؤْمِنُ ٱلْمُهَيْمِنُ ٱلْعَزِيزُ ٱلْجَبَّارُ ٱلْمُتَكَبِّرُ ۚ سُبْحَـٰنَ ٱللَّهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ۝٢٣

    Huwa Allahu allathee la ilaha illa huwa almaliku alquddoosu alssalamu almuminu almuhayminu alʿazeezu aljabbaru almutakabbiru subhana Allahi ʿamma yushrikoona

    Yeye ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye tu. Mfalme, Mtakatifu, Mwenye salama, Mtoaji wa amani, Mwenye kuyaendesha Mwenyewe mambo yake, Mwenye nguvu, Anaye fanya analo litaka, Mkubwa, Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo mshirikisha nayo.23

    Maelezo
    [23] Yeye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye, Mwenye kumiliki kila kitu kwa hakika, Aliye safika na kila upungufu, Aliye takasika na kila lisio mwelekea, Mwenye kusalimika na yote ya upungufu, Mwenye kuwaamini na kuwasadiki Mitume wake aliyo wapa nguvu kwa miujiza, Mlinzi Mwenye kuangalia kila kitu, Mwenye kushinda basi hashindwi na chochote, Mkubwa wa shani katika nguvu na utawala, Mwenye kutukuka na kila kisicho kuwa laiki na uzuri wake na utukufu wake, Mwenyezi Mungu ametakasika na hayo wanayo mshirikisha nayo.
  24. هُوَ ٱللَّهُ ٱلْخَـٰلِقُ ٱلْبَارِئُ ٱلْمُصَوِّرُ ۖ لَهُ ٱلْأَسْمَآءُ ٱلْحُسْنَىٰ ۚ يُسَبِّحُ لَهُۥ مَا فِى ٱلسَّمَـٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضِ ۖ وَهُوَ ٱلْعَزِيزُ ٱلْحَكِيمُ۝٢٤

    Huwa Allahu alkhaliqu albario almusawwiru lahu alasmao alhusna yusabbihu lahu ma fee alssamawati waalardi wahuwa alʿazeezu alhakeemu

    Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Muumbaji, Mtengenezaji, Mtia sura, Mwenye majina mazuri kabisa. Kila kilioko katika mbingu na ardhi kinamtakasa, naye ni Mwenye kushinda, Mwenye hikima.24

    Maelezo
    [24] Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Mwenye kuviumba vitu vyote tangu mwanzo bila ya ruwaza ya kuigia iliyo tangulia, Mwenye kuvipa sura kama vilivyo kwa mujibu wa atakavyo Yeye. Yeye ndiye Mwenye Majina Mazuri, Mwenye kutakaswa na kila kisicho kuwa laiki yake na kila kilichoko katika mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye kushinda, asiye shindwa na kitu. Mwenye hikima katika kupanga kwake na sharia zake.

Maswali yanayoulizwa mara kwa mara

Surat Al-Hashr maana yake ni nini?

Al-Hashr maana yake ni “Uhamisho”.

Surat Al-Hashr iko katika juzuu ya ngapi?

Surat Al-Hashr iko katika juzuu ya 28.

Surat Al-Hashr ina aya ngapi?

Surat Al-Hashr ina aya 24.

Surat Al-Hashr ni ya Makka au ya Madina?

Surat Al-Hashr ni sura ya Madina.

Surat Al-Hashr ni sura ya ngapi katika Qur’ani?

Ni sura ya 59 katika Qur’ani.

Vyanzo

  • Arabic text: Tanzil Quran Text (Uthmani) (Tanzil Project, CC BY 3.0), reproduced without changes.
  • Translation: Ali Muhsin Al-Barwani, from QuranEnc.com, version 1.0.1, reproduced without changes.
  • Transliteration: Tanzil.net English transliteration.
  • Recitation: Mishary Rashid Alafasy, via QuranicAudio.com and EveryAyah.com.
  • Word by word: recordings and meanings from Quran.com (Quran Foundation), played when you tap a word.
  • Madinah and IndoPak fonts (Settings): the text in those scripts and their fonts come from the Quran Foundation (Quran.com); the Madinah font is the King Fahd Glorious Quran Printing Complex's Uthmanic Hafs font.

Found a mistake? Report a mistake and we will check it against the source.

Mipangilio ya kusoma

Fonti ya Qur’ani
Ukubwa wa Kiarabu
100%
Ukubwa wa tafsiri
100%
Mandhari

Ongeza kwenye skrini ya kwanza

ReadSurahFungua ReadSurah kutoka skrini ya kwanza, kwa skrini nzima. Sura ulizosoma hufunguka hata bila intaneti.

  1. Katika Safari, gusa kitufe cha kushiriki (Share). Kwenye iPhone mpya kiko kwenye menyu ya •••.
  2. Gusa “Add to Home Screen”. Huenda ukahitaji kusogeza chini.
  3. Gusa “Add”.