سورة الحجر

Surat Al-Hijr kwa Kiswahili

Eneo la Miamba

Msahafu

Mishary Rashid AlafasyPakua MP3Pakua PDF

Surat Al-Hijr (الحجر) ni sura ya 15 katika Qur’ani na ina aya 99. Jina lake lina maana ya “Eneo la Miamba”. Ni sura ya Makka, iliyoteremshwa Makka kabla ya Hijra, na iko katika juzuu ya 14.

Katika ukurasa huu unaweza kusoma Surat Al-Hijr yote kwa Kiarabu, pamoja na tafsiri ya Kiswahili ya Ali Muhsin Al-Barwani aya kwa aya na matamshi kwa herufi za Kilatini, na kusikiliza kisomo chake.

Surat Al-Hijr kamili: Kiarabu, tafsiri ya Kiswahili na matamshi

بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَـٰنِ ٱلرَّحِيمِ

  1. الٓر ۚ تِلْكَ ءَايَـٰتُ ٱلْكِتَـٰبِ وَقُرْءَانٍ مُّبِينٍ۝١

    Aliflamra tilka ayatu alkitabi waquranin mubeenin

    Alif Lam Ra. (A.L.R). Hizi ni Aya za Kitabu na Qur'ani inayo bainisha.1

    Maelezo
    [1] Hizi ni Aya za Kitabu cha kusomwa, chenye kubainisha, chenye kuweke wazi.
  2. رُّبَمَا يَوَدُّ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ لَوْ كَانُوا۟ مُسْلِمِينَ۝٢

    Rubama yawaddu allatheena kafaroo law kanoo muslimeena

    HUENDA ikawa walio kufuru wakatamani wange kuwa Waislamu.2

    Maelezo
    [2] Watapenda, na watatamani sana makafiri wanao zikanya Aya za Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la, watapo ona adhabu ya Siku ya Kiyama, lau kuwa walisilimu walipo kuwapo duniani, na wakafuata kwa ikhlasi Dini ya Mwenyezi Mungu.
  3. ذَرْهُمْ يَأْكُلُوا۟ وَيَتَمَتَّعُوا۟ وَيُلْهِهِمُ ٱلْأَمَلُ ۖ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ۝٣

    Tharhum yakuloo wayatamattaʿoo wayulhihimu alamalu fasawfa yaʿlamoona

    Waache wale, na wastarehe, na iwazuge tamaa. Watakuja jua.3

    Maelezo
    [3] Lakini sasa wamo katika kughafilika, hawazingatii adhabu itakayo wapata Akhera! Basi ukisha wafikishia ujumbe wako, na ukawaonya, waachilie mbali. Wao hawana hamu ila kula, na kustarehe kwa ladha za dunia. Tamaa ya uwongo inawazuga. Na hakika bila ya shaka yoyote watakuja jua yatakayo wapata pale watapo yaona kwa macho yao Siku ya Kiyama.
  4. وَمَآ أَهْلَكْنَا مِن قَرْيَةٍ إِلَّا وَلَهَا كِتَابٌ مَّعْلُومٌ۝٤

    Wama ahlakna min qaryatin illa walaha kitabun maʿloomun

    Na hatukuuangamiza mji wowote ule ila ulikuwa na muda wake maalumu.4

    Maelezo
    [4] Na ikiwa wao wanataka wateremshiwe adhabu ya duniani, kama Mwenyezi Mungu alivyo wateketeza walio kuwa kabla yao, basi wajue kuwa Mwenyezi Mungu hauteketezi mji wowote ila kwa wakati wake maalumu.
  5. مَّا تَسْبِقُ مِنْ أُمَّةٍ أَجَلَهَا وَمَا يَسْتَـْٔخِرُونَ۝٥

    Ma tasbiqu min ommatin ajalaha wama yastakhiroona

    Hawawezi watu wowote kuitangulia ajali yao, wala kuchelewa.5

    Maelezo
    [5] Hawatangulii wala hawataakhari.
  6. وَقَالُوا۟ يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِى نُزِّلَ عَلَيْهِ ٱلذِّكْرُ إِنَّكَ لَمَجْنُونٌ۝٦

    Waqaloo ya ayyuha allathee nuzzila ʿalayhi alththikru innaka lamajnoonun

    Na walisema: Ewe uliyeteremshiwa Ukumbusho! Hakika wewe ni mwendawazimu.6

    Maelezo
    [6] Na uovu wa hali yao na wingi wa kughafilika kwao hata imefika hadi kumuita Nabii wao kwa kejeli wakisema: Ewe uliye teremshiwa Kitabu cha kukumbusha! Hapana shaka kuwa wewe una wazimu moja kwa moja! Huko kumuita kuwa ndiye aliye teremshiwa Ukumbusho, yaani Mawaidha, hakukuwa ila ni kwa kejeli tu, kumfanyia maskhara.
  7. لَّوْ مَا تَأْتِينَا بِٱلْمَلَـٰٓئِكَةِ إِن كُنتَ مِنَ ٱلصَّـٰدِقِينَ۝٧

    Law ma tateena bialmalaikati in kunta mina alssadiqeena

    Mbona hutuletei Malaika ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli?7

    Maelezo
    [7] Na hadi ya ukafiri wao walizidisha juu ya matusi hayo na kejeli kwa kusema: Laiti badala ya hicho Kitabu kilicho teremshwa ungeli tuletea Malaika wakawa ndio hoja yenyewe, kama wewe ni msema kweli miongoni mwa wenye kusema kweli!
  8. مَا نُنَزِّلُ ٱلْمَلَـٰٓئِكَةَ إِلَّا بِٱلْحَقِّ وَمَا كَانُوٓا۟ إِذًا مُّنظَرِينَ۝٨

    Ma nunazzilu almalaikata illa bialhaqqi wama kanoo ithan munthareena

    Sisi hatuwateremshi Malaika ila kwa sababu ya haki, na hapo hawatapewa muhula.8

    Maelezo
    [8] Na Mwenyezi Mungu aliye tukuka neno lake aliwajibu: Sisi hatuwateremshi Malaika ila huwa pamoja nao Haki ya nguvu yenye kuthibiti ambayo haina njia ya kuikataa. Basi wakiikanya huwa tena hawapewi muhula wowote, bali huteremshiwa adhabu ya hapa hapa duniani hapo hapo!
  9. إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا ٱلذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُۥ لَحَـٰفِظُونَ۝٩

    Inna nahnu nazzalna alththikra wainna lahu lahafithoona

    Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutao ulinda.9

    Maelezo
    [9] Na hakika, kwa ajili ya kuwa Wito wa Nabii huyu kwendea Haki udumu mpaka Siku ya Kiyama, hatuwateremshi Malaika, bali tumewateremshia hii Qur'ani ambayo kukumbusha kwake kunaendelea daima dawamu. Na Sisi ndio wenye kuilinda isiingiliwe na mageuzo na mabadiliko yoyote mpaka kusimama Kiyama.
  10. وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ فِى شِيَعِ ٱلْأَوَّلِينَ۝١٠

    Walaqad arsalna min qablika fee shiyaʿi alawwaleena

    Na hakika tulikwisha watumia Mitume mataifa ya mwanzo.10

    Maelezo
    [10] Na ewe Mtume Muaminifu! Usihuzunike; kwani Sisi tuliwatuma Mitume kabla yako kwa mataifa ambao wameshikilia upotovu kama hao walivyo shikilia. Na wao wamepita pamoja na wa kale walio teketezwa kwa ukafiri wao!
  11. وَمَا يَأْتِيهِم مِّن رَّسُولٍ إِلَّا كَانُوا۟ بِهِۦ يَسْتَهْزِءُونَ۝١١

    Wama yateehim min rasoolin illa kanoo bihi yastahzioona

    Na hakuwafikia Mtume ila walimkejeli.11

    Maelezo
    [11] Wala mtindo wao hao walio watangulia kwa kushikilia upotovu haukuwa ila kuwafanyia maskhara Mitume wao, Mtume baada ya Mtume, kama wanavyo kufanyia kejeli wewe! Huo ndio mtindo wa wapotovu!
  12. كَذَٰلِكَ نَسْلُكُهُۥ فِى قُلُوبِ ٱلْمُجْرِمِينَ۝١٢

    Kathalika naslukuhu fee quloobi almujrimeena

    Na kama hivi ndivyo tunavyo ingiza katika nyoyo za wakosefu.12

    Maelezo
    [12] Kama tulivyo itia Qur'ani katika nyoyo za Waumini ikaingiza mwangaza, basi kadhaalika tumeingiza upotovu katika nyoyo za walio pigwa muhuri wa ukosefu; hali ya katika nyoyo zao ikawa kinyume cha hayo. Upotovu ukatia mizizi katika roho zao.
  13. لَا يُؤْمِنُونَ بِهِۦ ۖ وَقَدْ خَلَتْ سُنَّةُ ٱلْأَوَّلِينَ۝١٣

    La yuminoona bihi waqad khalat sunnatu alawwaleena

    Hawayaamini haya, na hali ya kuwa umekwisha wapitia mfano wa watu wa kale.13

    Maelezo
    [13] Wakhalifu hao hawaamini. Na mwendo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwapa muhula mpaka waione adhabu chungu ya Siku ya Kiyama ndio kama ulivyo kwisha tangulia.
  14. وَلَوْ فَتَحْنَا عَلَيْهِم بَابًا مِّنَ ٱلسَّمَآءِ فَظَلُّوا۟ فِيهِ يَعْرُجُونَ۝١٤

    Walaw fatahna ʿalayhim baban mina alssamai fathalloo feehi yaʿrujoona

    Na lau tungeli wafungulia mlango wa mbingu, wakawa wanapanda,14

    Maelezo
    [14] Watu hao wanataka wateremshiwe Malaika. Ewe Nabii! Usidhani kuwa ndio wataamini wakiteremshiwa. Bali hata tungeli wafungulia mlango wa mbingu wakawa wanapanda huko wakaona maajabu yaliyoko, na wakawaona Malaika,
  15. لَقَالُوٓا۟ إِنَّمَا سُكِّرَتْ أَبْصَـٰرُنَا بَلْ نَحْنُ قَوْمٌ مَّسْحُورُونَ۝١٥

    Laqaloo innama sukkirat absaruna bal nahnu qawmun mashooroona

    Basi wangeli sema: Macho yetu yamelevywa, bali sisi wenyewe tumerogwa.15

    Maelezo
    [15] Bado wasingeli amini, na wangesema: Macho yetu yamefumbwa tusione, na yamefunikwa. Bali hayo si lolote ila ni uchawi tu, tumerogwa! Basi hapana faida ya ishara yoyote maadamu nyoyo zao zimeenea ukafiri.
  16. وَلَقَدْ جَعَلْنَا فِى ٱلسَّمَآءِ بُرُوجًا وَزَيَّنَّـٰهَا لِلنَّـٰظِرِينَ۝١٦

    Walaqad jaʿalna fee alssamai buroojan wazayyannaha lilnnathireena

    Na hakika tumeweka katika mbingu vituo vya sayari, na tumezipamba kwa wenye kuangalia.16

    Maelezo
    [16] Na Sisi tumeweka mbinguni sayari na nyota, kwa makundi yenye hisabu zake na yenye kukhitalifiana umbo lake na sura yake. Na kadhaalika tukazipamba kwa wenye kuziangalia kwa kutuza na kuzingatia, na kuchunguza kwazo dalili za uwezo wa Muumbaji wao.
  17. وَحَفِظْنَـٰهَا مِن كُلِّ شَيْطَـٰنٍ رَّجِيمٍ۝١٧

    Wahafithnaha min kulli shaytanin rajeemin

    Na tumezilinda na kila shetani afukuzwaye.17

    Maelezo
    [17] Lakini Sisi tumezihifadhi na kila shetani anaye stahiki kupigwa vimondo na kufukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
  18. إِلَّا مَنِ ٱسْتَرَقَ ٱلسَّمْعَ فَأَتْبَعَهُۥ شِهَابٌ مُّبِينٌ۝١٨

    Illa mani istaraqa alssamʿa faatbaʿahu shihabun mubeenun

    Isipo kuwa mwenye kusikiliza kwa kuibia, naye hufuatwa na kijinga cha moto kinacho onekana.18

    Maelezo
    [18] Na yeyote katika hao mashetani wanao jaribu kuibia kusikiliza maneno yanayo jiri baina ya wakaazi wa hizi nyote, basi Sisi tunampopoa kwa vijinga vya moto vya mbinguni vinavyo onekana wazi.
  19. وَٱلْأَرْضَ مَدَدْنَـٰهَا وَأَلْقَيْنَا فِيهَا رَوَٰسِىَ وَأَنۢبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ شَىْءٍ مَّوْزُونٍ۝١٩

    Waalarda madadnaha waalqayna feeha rawasiya waanbatna feeha min kulli shayin mawzoonin

    Na ardhi tumeitandaza na humo tumeweka milima, na tumeotesha kila kitu kwa kiasi chake.19

    Maelezo
    [19] Na tumekuumbieni ardhi, na tumekutengenezeeni mpaka ikawa kama busati lilio tandikwa, na tukaweka ndani yake milima iliyo simama imara. Na tumekuotesheeni ndani namna mbali mbali za mimea ya kukufaeni kwa uhai wenu, na tumeifanya kwa vipimo na zama maalumu katika kukua kwake, na faida yake kwa kula, na kwa kadiri ya haja zenu na kwa vipimo vyake, na sura yake kwa umbo na tabia. Aya hii inaeleza uhakika wa uumbaji ambao haukujuulikana ila katika zama za hivi karibuni. Nayo ni kuwa kila kabila ya mimea imefanana kati yao kwa kuonekana na undani wake, hata katika sehemu zake ndogo ndogo, katika viungo vyake vyote vya hiyo mimea. Na hali kadhaalika katika "Khalaya" au "Cells" za hiyo mimea ya kabila fulani, kwa ajili ya kutimiza kazi iliyo kusudiwa kiungo hicho cha mmea. Na pia sehemu za mimea ya hizo kabila zao na vilivyo undwa katika viungo vyake utaona mnasaba wake umethibiti kila mwaka, ukilinganisha kwa wakati ule ule katika miaka mingine
  20. وَجَعَلْنَا لَكُمْ فِيهَا مَعَـٰيِشَ وَمَن لَّسْتُمْ لَهُۥ بِرَٰزِقِينَ۝٢٠

    Wajaʿalna lakum feeha maʿayisha waman lastum lahu biraziqeena

    Na tumekujaalieni humo vitu vya maisha yenu, na ya hao ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku.20

    Maelezo
    [20] Na tumekujaalieni katika ardhi sababu za maisha mema. Kwani ndani yake yamo mawe ya kujengea majumba, na wanyama mnao nafiika kwa nyama yao, au ngozi zao, au manyoa yao. Na yapo maadeni yanayo toka chini ya ardhi, na mengineyo. Kama ilivyo kuwa humo zipo sababu za kukuleteeni nyinyi maisha mema, basi humo pia wanapata maisha wenginewe ambao wapo chini ya mamlaka yenu, kama watoto na wafwasi, ambao Mwenyezi Mungu pekee ndiye anaye waruzuku wao na nyinyi.
  21. وَإِن مِّن شَىْءٍ إِلَّا عِندَنَا خَزَآئِنُهُۥ وَمَا نُنَزِّلُهُۥٓ إِلَّا بِقَدَرٍ مَّعْلُومٍ۝٢١

    Wain min shayin illa ʿindana khazainuhu wama nunazziluhu illa biqadarin maʿloomin

    Na hakuna chochote ila asili yake inatokana na Sisi; wala hatukiteremshi ila kwa kipimo maalumu.21

    Maelezo
    [21] Na hapana chochote cha kheri ila kiko kwetu kama mahodhi yaliyo jaa, nasi tunakiweka tayari na tunakitoa kwa wakati wake. Na hatuwateremshii waja wetu ila kwa kiasi maalumu, kwa mujibu tunavyo pima kwa hikima yetu ya maumbile.
  22. وَأَرْسَلْنَا ٱلرِّيَـٰحَ لَوَٰقِحَ فَأَنزَلْنَا مِنَ ٱلسَّمَآءِ مَآءً فَأَسْقَيْنَـٰكُمُوهُ وَمَآ أَنتُمْ لَهُۥ بِخَـٰزِنِينَ۝٢٢

    Waarsalna alrriyaha lawaqiha faanzalna mina alssamai maan faasqaynakumoohu wama antum lahu bikhazineena

    Na tunazipeleka pepo za kupandishia, na tunateremsha kutoka mbinguni maji, kisha tukakunywesheni maji hayo. Wala si nyinyi mnayo yaweka.22

    Maelezo
    [22] Na Sisi tulipeleka pepo zilizo beba mvua na zilizo beba mbegu za mimea, na tukateremsha maji ya kukunywesheni. Na hayo ni kwa kufuata vile tutakavyo. Na yeyote yule hawezi kuyatenda kama hayo ila awe nayo kwake kama mahodhi au mabirika. Aya hii imeitangulia sayansi kwa kusema kuwa upepo unafanya kazi kubwa katika kubeba pollen, chembe dume za kupandishia mimea, kupelekea sehemu za uke za mimea mingine, na kwa hivyo yakazalikana mazao. Na pia haikujuulikana ila mwanzo wa karne hii tuliyo nayo kwamba upepo unazalisha mawingu yanayo nyesha mvua. Kwani "Nucleons" ambazo juu yake hujumuika sehemu za mvuke wa maji na zikawa chembe chembe za maji ndani ya wingu, ndizo chanzo cha mvua inayo chukuliwa na pepo kupelekwa kwenye majimbo yanayo fikiwa na mawingu. Misingi ya hizo "Nucleons" ni chumvi ya bahari, na vinavyo chukuliwa na upepo juu ya uso wa ardhi, na "Oxides" na vumbi vumbi, n.k. Na vyote hivyo ni lazima kwa ajili ya mvua. "Wala si nyinyi mnayo yaweka". Imethibiti kwa sayansi ya kisasa kuwa mvua inaanza kwa mvuke kutokana na uso wa ardhi na bahari, kisha inarejea hali ile ile tena kama ilivyo tajwa. Ikinya mvua hunywesha kila kilicho na uhai katika ardhi, na huinywesha ardhi yenyewe. Wala haiwezekani kuzuilika, kwa sababu ikichuruzika kutokana na vyote vyenye uhai na katika ardhi ikaingia baharini, tena kisha huanza kuzunguka mara ya pili kwa kupanda mvuke kutoka baharini. Basi hali ni hivyo mzunguko. Hapa ndio inabainika maana ya Aya "Wala si nyinyi mnayo yaweka."
  23. وَإِنَّا لَنَحْنُ نُحْىِۦ وَنُمِيتُ وَنَحْنُ ٱلْوَٰرِثُونَ۝٢٣

    Wainna lanahnu nuhyee wanumeetu wanahnu alwarithoona

    Na Sisi ndio tunao huisha na tunao fisha. Na Sisi ndio Warithi.23

    Maelezo
    [23] Na ni Sisi tu peke yetu ndio tunavipa vitu vyote uhai, kisha tunavipelekea mauti, kwani uumbaji wote ni wetu.
  24. وَلَقَدْ عَلِمْنَا ٱلْمُسْتَقْدِمِينَ مِنكُمْ وَلَقَدْ عَلِمْنَا ٱلْمُسْتَـْٔخِرِينَ۝٢٤

    Walaqad ʿalimna almustaqdimeena minkum walaqad ʿalimna almustakhireena

    Na tunawajua walio tangulia katika nyinyi, na tunawajua waliotaakhari.24

    Maelezo
    [24] Na kila mmoja wenu ana muda wake alio pimiwa. Sisi ndio tunao ujua. Tunawajua walio tangulia kwa kufa na kuwa hai, na pia wanao taakhari.
  25. وَإِنَّ رَبَّكَ هُوَ يَحْشُرُهُمْ ۚ إِنَّهُۥ حَكِيمٌ عَلِيمٌ۝٢٥

    Wainna rabbaka huwa yahshuruhum innahu hakeemun ʿaleemun

    Na hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye wakusanya. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mjuzi.25

    Maelezo
    [25] Na hakika walio tangulia na walio taakhari watakusanywa wakati mmoja. Na Mwenyezi Mungu atawahisabia na atawalipa. Na hayo ni kwa mujibu wa hikima yake na ujuzi wake. Na Yeye ndiye anaye itwa Mwenye hikima, Mwenye ujuzi.
  26. وَلَقَدْ خَلَقْنَا ٱلْإِنسَـٰنَ مِن صَلْصَـٰلٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ۝٢٦

    Walaqad khalaqna alinsana min salsalin min hamain masnoonin

    Na tulimuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura.26

    Maelezo
    [26] Na Sisi katika kuumba kwetu walimwengu katika dunia hii, tumeumba namna mbili - Tumemuumba mtu kwa udongo mkavu wenye kutoa sauti ukigongwa.
  27. وَٱلْجَآنَّ خَلَقْنَـٰهُ مِن قَبْلُ مِن نَّارِ ٱلسَّمُومِ۝٢٧

    Waaljanna khalaqnahu min qablu min nari alssamoomi

    Na majini tuliwaumba kabla kwa moto wa upepo umoto.27

    Maelezo
    [27] Na makhaluku wengine ni majini, ambao tuliwaumba mbele, alipo umbwa asili yake Iblisi kutokana na moto mkali mno unao toka katika tundu za mwili wa mtu.
  28. وَإِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلَـٰٓئِكَةِ إِنِّى خَـٰلِقٌۢ بَشَرًا مِّن صَلْصَـٰلٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ۝٢٨

    Waith qala rabbuka lilmalaikati innee khaliqun basharan min salsalin min hamain masnoonin

    Na Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Hakika Mimi nitamuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura.28

    Maelezo
    [28] Ewe Nabii! Kumbuka asli ya viumbe. Pale alipo sema Aliye kuumba, Mola Mlezi wa viumbe vyote, kuwaambia Malaika: Mimi nataka kumuanzisha mtu niliye muumba kutokana na udongo mkavu, wenye kutoa sauti ukigongwa, nao umebadilika rangi, na una sura.
  29. فَإِذَا سَوَّيْتُهُۥ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِن رُّوحِى فَقَعُوا۟ لَهُۥ سَـٰجِدِينَ۝٢٩

    Faitha sawwaytuhu wanafakhtu feehi min roohee faqaʿoo lahu sajideena

    Basi nitakapo mkamilisha na nikampulizia roho yangu, basi mumwangukie kumsujudia.29

    Maelezo
    [29] Nikisha kamilisha kumuumba, na nikampulizia roho ambayo ninaimiliki, basi teremkeni kwa nyuso zenu mkimsujudia, kwa kumwamkia na kumhishimu.
  30. فَسَجَدَ ٱلْمَلَـٰٓئِكَةُ كُلُّهُمْ أَجْمَعُونَ۝٣٠

    Fasajada almalaikatu kulluhum ajmaʿoona

    Basi Malaika wote pamoja walimsujudia,30

    Maelezo
    [30] Wakasujudu wote kwa kuit'ii amri ya Mwenyezi Mungu.
  31. إِلَّآ إِبْلِيسَ أَبَىٰٓ أَن يَكُونَ مَعَ ٱلسَّـٰجِدِينَ۝٣١

    Illa ibleesa aba an yakoona maʿa alssajideena

    Isipo kuwa Iblisi. Yeye alikataa kuwa pamoja na walio sujudu.31

    Maelezo
    [31] Lakini Iblisi alijivuna na akakataa kuwa pamoja na Malaika waliyo it'ii amri ya Mwenyezi Mungu.
  32. قَالَ يَـٰٓإِبْلِيسُ مَا لَكَ أَلَّا تَكُونَ مَعَ ٱلسَّـٰجِدِينَ۝٣٢

    Qala ya ibleesu ma laka alla takoona maʿa alssajideena

    (Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Iblisi! Una nini hata hukuwa pamoja na walio sujudu?32

    Maelezo
    [32] Hapo basi Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema: Ewe Iblisi! Kitu gani kilicho kupelekea hata ukaasi na usiwe pamoja na wanyenyekevu walio sujudu?
  33. قَالَ لَمْ أَكُن لِّأَسْجُدَ لِبَشَرٍ خَلَقْتَهُۥ مِن صَلْصَـٰلٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ۝٣٣

    Qala lam akun liasjuda libasharin khalaqtahu min salsalin min hamain masnoonin

    Akasema: Haiwi mimi nimsujudie mtu uliye muumba kwa udongo unaotoa sauti, unao tokana na matope yenye sura.33

    Maelezo
    [33] Iblisi akasema: Si shani yangu mimi kumsujudia mtu uliye muumba kwa udongo mkavu, wenye kutoa sauti ukigongwa, nao umegeuka rangi, wenye kutiwa sura.
  34. قَالَ فَٱخْرُجْ مِنْهَا فَإِنَّكَ رَجِيمٌ۝٣٤

    Qala faokhruj minha fainnaka rajeemun

    (Mwenyezi Mungu) akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe ni maluuni!34

    Maelezo
    [34] Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: Ukiwa wewe umekuwa a'asi, umetokana na ut'iifu wangu, basi tokelea mbali kwenye Bustani hii! Kwani hakika wewe umefukuzwa kwenye rehema yangu pahala pa hishima.
  35. وَإِنَّ عَلَيْكَ ٱللَّعْنَةَ إِلَىٰ يَوْمِ ٱلدِّينِ۝٣٥

    Wainna ʿalayka allaʿnata ila yawmi alddeeni

    Na hakika juu yako ipo laana mpaka Siku ya Malipo.35

    Maelezo
    [35] Na Mimi nimekwisha kuhukumia ubaidike na rehema na utukufu mpaka Siku ya Kiyama, Siku ya Hisabu na Malipo. Na hapo ndipo utapo pata adhabu, wewe na wanao kufuata .
  36. قَالَ رَبِّ فَأَنظِرْنِىٓ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ۝٣٦

    Qala rabbi faanthirnee ila yawmi yubʿathoona

    Akasema (Iblisi): Mola wangu Mlezi! Nipe muhula mpaka siku watapofufuliwa.36

    Maelezo
    [36] Iblisi akasema, hali naye kesha kuwa ni mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu: Ewe Muumba wangu! Nipe muhula, nibakishe usinitwae mpaka Siku ya Kiyama, Siku watapo fufuliwa watu wakawa hai baada ya kufa kwao.
  37. قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ ٱلْمُنظَرِينَ۝٣٧

    Qala fainnaka mina almunthareena

    (Mwenyezi Mungu) akasema: Hakika wewe ni katika walio pewa muhula37

    Maelezo
    [37] Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: Wewe utabakishwa, umepewa muhula,
  38. إِلَىٰ يَوْمِ ٱلْوَقْتِ ٱلْمَعْلُومِ۝٣٨

    Ila yawmi alwaqti almaʿloomi

    Mpaka siku ya wakati maalumu.38

    Maelezo
    [38] Mpaka wakati niliyo ukadiria, ninao ujua Mimi. Na kama utavyo kuwa mrefu una kikomo.
  39. قَالَ رَبِّ بِمَآ أَغْوَيْتَنِى لَأُزَيِّنَنَّ لَهُمْ فِى ٱلْأَرْضِ وَلَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ۝٣٩

    Qala rabbi bima aghwaytanee laozayyinanna lahum fee alardi walaoghwiyannahum ajmaʿeena

    Akasema: Mola wangu Mlezi! Ilivyo kuwa umenitia makosani, basi nahakikisha nitawazaini hapa duniani na nitawapoteza wote,39

    Maelezo
    [39] Akasema Iblisi, mkhalifu, a'asi: Ewe Muumba wangu unaye nibakisha! Umenitakia upotofu, nami nikatumbukia ndani yake. Basi kwa sababu hiyo nahakikisha kuwa nitawapambia wanaadamu maovu wayaone mazuri, na nitafanya kila juhudi kuwapotoa wote!
  40. إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ ٱلْمُخْلَصِينَ۝٤٠

    Illa ʿibadaka minhumu almukhlaseena

    Ila waja wako walio safika.40

    Maelezo
    [40] Wala hawatoepukana na upotovu wangu ila wale waja wako walio kufanyia ikhlasi Wewe na nisio weza kuzimiliki nyoyo zao kwa zilivyo kuwa imara kwa kukumbuka Wewe.
  41. قَالَ هَـٰذَا صِرَٰطٌ عَلَىَّ مُسْتَقِيمٌ۝٤١

    Qala hatha siratun ʿalayya mustaqeemun

    Akasema: Hii Njia ya kujia kwangu Iliyo Nyooka.41

    Maelezo
    [41] Hakika usafi wa waja walio isafia niya Dini yao ndio Njia Iliyo Nyooka, na haki yangu nisiikiuke, kwani hao siwezi kuwapotoa. (Tafsiri hii yaonyesha maneno hayo ni ya Iblisi. Lakini Tafsiri nyengine zinasema maneno hayo ni ya Mwenyezi Mungu, kwa mfano ya Abdulla Saleh, Abdulla Yusuf, Pickthall, Razi, Baidhawi, Qurtubi, Zamakhshari, Ibn Kathir, Assad.)
  42. إِنَّ عِبَادِى لَيْسَ لَكَ عَلَيْهِمْ سُلْطَـٰنٌ إِلَّا مَنِ ٱتَّبَعَكَ مِنَ ٱلْغَاوِينَ۝٤٢

    Inna ʿibadee laysa laka ʿalayhim sultanun illa mani ittabaʿaka mina alghaweena

    Hakika waja wangu, wewe hutakuwa na mamlaka juu yao, isipo kuwa wale wapotofu walio kufuata.42

    Maelezo
    [42] Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: Hakika waja wangu walio nisafia Mimi Dini yao wewe huna uwezo wa kuwapoteza. Lakini wapotovu, walio zama katika upotovu, walio kufuata wewe, basi hao ndio unayo madaraka juu ya nyoyo zao.
  43. وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمَوْعِدُهُمْ أَجْمَعِينَ۝٤٣

    Wainna jahannama lamawʿiduhum ajmaʿeena

    Na bila shaka Jahannamu ndipo pahali pao walipo ahidiwa wote.43

    Maelezo
    [43] Na hakika Moto mkali mno ndio wameahidiwa hao wote kuwa ndiyo adhabu ya kutia uchungu.
  44. لَهَا سَبْعَةُ أَبْوَٰبٍ لِّكُلِّ بَابٍ مِّنْهُمْ جُزْءٌ مَّقْسُومٌ۝٤٤

    Laha sabʿatu abwabin likulli babin minhum juzon maqsoomun

    Ina milango saba; na kwa kila mlango iko sehemu walio tengewa.44

    Maelezo
    [44] Wala huo Moto mkali hauna mlango mmoja tu, bali una milango saba kwa ajili ya wingi wanao stahiki kuingia humo. Na kila mlango una kundi lake makhsusi. Na kila kundi una cheo chake maalumu cha kulingana na uovu wake.
  45. إِنَّ ٱلْمُتَّقِينَ فِى جَنَّـٰتٍ وَعُيُونٍ۝٤٥

    Inna almuttaqeena fee jannatin waʿuyoonin

    Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem.45

    Maelezo
    [45] Haya ni malipo ya wanao mfuata Shetani. Ama wale ambao Shetani kashindwa kuwapotoa, kwa kuwa wameweka kinga baina yake na nyoyo zao, hao watapata Mabustani yaliyo bora, na chemchem zinazo pita .
  46. ٱدْخُلُوهَا بِسَلَـٰمٍ ءَامِنِينَ۝٤٦

    Odkhulooha bisalamin amineena

    (Wataambiwa:) Ingieni kwa salama na amani.46

    Maelezo
    [46] Mola wao Mlezi atawaambia: Ingieni katika Bustani hizi kwa utulivu na amani. Kwani hapana khofu juu yenu, hamhuzunikii nyakati zenu.
  47. وَنَزَعْنَا مَا فِى صُدُورِهِم مِّنْ غِلٍّ إِخْوَٰنًا عَلَىٰ سُرُرٍ مُّتَقَـٰبِلِينَ۝٤٧

    Wanazaʿna ma fee sudoorihim min ghillin ikhwanan ʿala sururin mutaqabileena

    Na tutaondoa chuki iliyo kuwamo vifuani mwao, wawe ndugu juu ya viti vya enzi wameelekeana.47

    Maelezo
    [47] Na hakika watu wa Imani wataishi katika kheri hii na nafsi zao zimetua. Kwani tumezitoa chuki zilizo kuwamo katika nafsi hizo. Wote hao watakuwa ndugu waketi juu ya viti vya enzi zikitazamana nyuso zao kwa furaha na mahaba, wala hawawi mmoja nyuma ya mwenzie wakichunguliana visogoni.
  48. لَا يَمَسُّهُمْ فِيهَا نَصَبٌ وَمَا هُم مِّنْهَا بِمُخْرَجِينَ۝٤٨

    La yamassuhum feeha nasabun wama hum minha bimukhrajeena

    Humo hayatawagusa machofu, wala hawatatolewa humo.48

    Maelezo
    [48] Hawapatwi na machofu huko. Na hiyo ni neema ya daima, wala hawatotoka humo milele.
  49. ۞ نَبِّئْ عِبَادِىٓ أَنِّىٓ أَنَا ٱلْغَفُورُ ٱلرَّحِيمُ۝٤٩

    Nabbi ʿibadee annee ana alghafooru alrraheemu

    Waambie waja wangu ya kwamba Mimi ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.49

    Maelezo
    [49] Ewe Nabii muaminifu! Wape khabari waja wangu wote kwamba Mimi ni Mwingi wa kughufiria na kusamehe kwa mwenye kutubu, akaamini, na akatenda mema. Na kwamba Mimi ni Mwingi wa kuwarehemu.
  50. وَأَنَّ عَذَابِى هُوَ ٱلْعَذَابُ ٱلْأَلِيمُ۝٥٠

    Wa anna ʿathabee huwa alʿathabu alaleemu

    Na kwamba adhabu yangu ndio adhabu iliyo chungu!50

    Maelezo
    [50] Na wape khabari kwamba adhabu ninayo wateremshia wenye kuasi na kukufuru ni adhabu yenye kutia machungu kweli, na adhabu yoyote nyengineyo haihisabiwi kuwa ina machungu mbele ya hii.
  51. وَنَبِّئْهُمْ عَن ضَيْفِ إِبْرَٰهِيمَ۝٥١

    Wanabbihum ʿan dayfi ibraheema

    Na uwape khabari za wageni wa Ibrahim.51

    Maelezo
    [51] Ewe Nabii! Waambie pia, katika kubainisha rehema yangu makhsusi katika dunia na adhabu yangu kwa wenye kuasi humo, khabari ya Malaika walio mfikia Ibrahim kama wageni.
  52. إِذْ دَخَلُوا۟ عَلَيْهِ فَقَالُوا۟ سَلَـٰمًا قَالَ إِنَّا مِنكُمْ وَجِلُونَ۝٥٢

    Ith dakhaloo ʿalayhi faqaloo salaman qala inna minkum wajiloona

    Walipo ingia kwake na wakasema: Salama! Yeye akasema: Hakika sisi tunakuogopeni.52

    Maelezo
    [52] Ewe Muaminifu! Watajie pale walipo ingia kwake, naye akawaogopa. Wao wakamwambia: Amani kwako, na tulia! Yeye akasema: Sisi tunakuogopeni, kwani mmetujia kwa ghafla, sio wakati wa dasturi wa kufika wageni, na hatujui mna nini!
  53. قَالُوا۟ لَا تَوْجَلْ إِنَّا نُبَشِّرُكَ بِغُلَـٰمٍ عَلِيمٍ۝٥٣

    Qaloo la tawjal inna nubashshiruka bighulamin ʿaleemin

    Wakasema: Usiogope. Sisi tunakubashiria kijana mwenye ujuzi.53

    Maelezo
    [53] Wakasema: Usiogope, na tuwa moyo! Kwani tunakubashiria mwana, ambaye Mwenyezi Mungu Mtukufu atampa siku zijazo za uhai wake ilimu kubwa. Inaonyesha hapa kuwa bishara hii si ya Ismail a.s. Kwani Ismail alikuwa kesha zaliwa, naye na mama yake Haajir walikuwa wapo Makka. Bishara hii ni ya Ibrahim na mkewe, basi kwa hivyo ni ya Is-haq mwana wa Ibrahim na Sara.
  54. قَالَ أَبَشَّرْتُمُونِى عَلَىٰٓ أَن مَّسَّنِىَ ٱلْكِبَرُ فَبِمَ تُبَشِّرُونَ۝٥٤

    Qala abashshartumoonee ʿala an massaniya alkibaru fabima tubashshirooni

    Akasema: Mnanibashiria nami uzee umenishika! Basi kwa njia gani mnanibashiria?54

    Maelezo
    [54] Akasema: Vipi mnanibashiria mtoto na hali mimi nimekwisha patikana na udhaifu wa ukongwe. Kwa njia gani, basi, mnanibashiria jambo hili la ajabu?
  55. قَالُوا۟ بَشَّرْنَـٰكَ بِٱلْحَقِّ فَلَا تَكُن مِّنَ ٱلْقَـٰنِطِينَ۝٥٥

    Qaloo bashsharnaka bialhaqqi fala takun mina alqaniteena

    Wakasema: Tunakubashiria kwa haki; basi usiwe miongoni mwa wanaokata tamaa.55

    Maelezo
    [55] Wakasema: Sisi tunakubashiria jambo lilio thibiti, ambalo halina shaka kabisa. Basi usiwe katika wanao kata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu.
  56. قَالَ وَمَن يَقْنَطُ مِن رَّحْمَةِ رَبِّهِۦٓ إِلَّا ٱلضَّآلُّونَ۝٥٦

    Qala waman yaqnatu min rahmati rabbihi illa alddalloona

    Akasema: Na nani anaye kata tamaa na rehema ya Mola wake Mlezi ila wale walio potea?56

    Maelezo
    [56] Ibrahim akasema: Mimi sikati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Kwani hawakati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu ila walio potea wasio utambua utukufu wake na uwezo wake.
  57. قَالَ فَمَا خَطْبُكُمْ أَيُّهَا ٱلْمُرْسَلُونَ۝٥٧

    Qala fama khatbukum ayyuha almursaloona

    Akasema: Hebu nini amri yenu, enyi wajumbe?57

    Maelezo
    [57] Alivyo kuwa kaanza kuzoeana nao, alisema: Ikiwa mmenibashiria khabari hii nzuri, je mna jambo gani jenginelo mlilo nalo baada ya haya, enyi wajumbe mlio tumwa na Mwenyezi Mungu?
  58. قَالُوٓا۟ إِنَّآ أُرْسِلْنَآ إِلَىٰ قَوْمٍ مُّجْرِمِينَ۝٥٨

    Qaloo inna orsilna ila qawmin mujrimeena

    Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya wakosefu!58

    Maelezo
    [58] Wakasema hakika sisi tumetumwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa watu walio fanya ukhalifu katika Haki ya Mwenyezi Mungu na haki ya Nabii wao, na haki ya nafsi zao wenyewe. Ukhalifu ndio mtindo wao. Watu wenyewe ni kaumu ya Luut'i. Basi tutawateketeza.
  59. إِلَّآ ءَالَ لُوطٍ إِنَّا لَمُنَجُّوهُمْ أَجْمَعِينَ۝٥٩

    Illa ala lootin inna lamunajjoohum ajmaʿeena

    Isipo kuwa walio mfuata Luut'i. Bila ya shaka sisi tutawaokoa hao wote.59

    Maelezo
    [59] Wala hakusalimika na huo ukhalifu na adhabu yake ila ahli zake yeye Luut'i. Basi hao Mwenyezi Mungu Mtukufu ametuamrisha tuwaokoe wote.
  60. إِلَّا ٱمْرَأَتَهُۥ قَدَّرْنَآ ۙ إِنَّهَا لَمِنَ ٱلْغَـٰبِرِينَ۝٦٠

    Illa imraatahu qaddarna innaha lamina alghabireena

    Ila mkewe. Tunakadiria huyo atakuwa miongoni watao bakia nyuma.60

    Maelezo
    [60] Na hatoangamia katika ahli zake ila mkewe, kwani yeye hakumfuata mumewe, bali yu pamoja na hao wakosefu ambao wanao stahiki adhabu.
  61. فَلَمَّا جَآءَ ءَالَ لُوطٍ ٱلْمُرْسَلُونَ۝٦١

    Falamma jaa ala lootin almursaloona

    Basi wale wajumbe walipo fika kwa Luut'i,61

    Maelezo
    [61] Wale Malaika walio tumwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kuteremsha yaliyo ahidiwa, walipo fika nchi ya Luut'i na watu wake,
  62. قَالَ إِنَّكُمْ قَوْمٌ مُّنكَرُونَ۝٦٢

    Qala innakum qawmun munkaroona

    Alisema (Luut'i): Hakika nyinyi ni watu msio juulikana.62

    Maelezo
    [62] Luut'i aliwaambia: Watu nyinyi sikujueni, na nafsi yangu inatishika nanyi. Naogopa msituletee balaa.
  63. قَالُوا۟ بَلْ جِئْنَـٰكَ بِمَا كَانُوا۟ فِيهِ يَمْتَرُونَ۝٦٣

    Qaloo bal jinaka bima kanoo feehi yamtaroona

    Wakasema: Bali sisi tumekuletea yale waliyo kuwa wakiyafanyia shaka.63

    Maelezo
    [63] Wakasema: Usituogope, kwani hatukukujia kwa unalo liogopa, bali tumekujia kwa jambo la kukufurahisha, nalo ni kuwateremshia adhabu hawa watu wako walio kukadhibisha na wakawa wanaitilia shaka hiyo adhabu au wanaikanya.
  64. وَأَتَيْنَـٰكَ بِٱلْحَقِّ وَإِنَّا لَصَـٰدِقُونَ۝٦٤

    Waataynaka bialhaqqi wainna lasadiqoona

    Na tumefika kwako kwa Haki, na hakika sisi tunasema kweli.64

    Maelezo
    [64] Nasi tumekujia kwa amri iliyo thaabiti isiyo na shaka, nayo ni kuiteremsha adhabu. Na kutimiza ahadi ni katika sifa yetu, kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
  65. فَأَسْرِ بِأَهْلِكَ بِقِطْعٍ مِّنَ ٱلَّيْلِ وَٱتَّبِعْ أَدْبَـٰرَهُمْ وَلَا يَلْتَفِتْ مِنكُمْ أَحَدٌ وَٱمْضُوا۟ حَيْثُ تُؤْمَرُونَ۝٦٥

    Faasri biahlika biqitʿin mina allayli waittabiʿ adbarahum wala yaltafit minkum ahadun waimdoo haythu tumaroona

    Basi ondoka na ahli zako usiku ungalipo, nawe ufuate nyuma yao,wala yeyote kati yenu asigeuke nyuma. Na mwende mnapo amrishwa.65

    Maelezo
    [65] Ilivyo kuwa adhabu itawateremkia, basi wewe na ahli zako mlio andikiwa kuokoka, tokeni baada ya kwisha ingia usiku.
  66. وَقَضَيْنَآ إِلَيْهِ ذَٰلِكَ ٱلْأَمْرَ أَنَّ دَابِرَ هَـٰٓؤُلَآءِ مَقْطُوعٌ مُّصْبِحِينَ۝٦٦

    Waqadayna ilayhi thalika alamra anna dabira haolai maqtooʿun musbiheena

    Na tukamfunulia hukumu hiyo, ya kwamba hata wa mwisho wao hao ikifika asubuhi atakuwa kesha katiliwa mbali.66

    Maelezo
    [66] Na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la alimfunulia Luut'i kwa kumwambia: Sisi tumewahukumia na kuwakadiria wakosefu kuteketea. Watang'olewa itapoingia asubuhi, wala hatobaki hata mmoja wao.
  67. وَجَآءَ أَهْلُ ٱلْمَدِينَةِ يَسْتَبْشِرُونَ۝٦٧

    Wajaa ahlu almadeenati yastabshiroona

    Na wakaja watu wa mji ule nao furahani.67

    Maelezo
    [67] Asubuhi kulipo pambazuka waliwaona Malaika kwa sura ya binaadamu wazuri. Wao wale wakawafurahia, wakaja ili wafanye nao vitendo vyao viovu, vya kuwaingilia wanaume.
  68. قَالَ إِنَّ هَـٰٓؤُلَآءِ ضَيْفِى فَلَا تَفْضَحُونِ۝٦٨

    Qala inna haolai dayfee fala tafdahooni

    Akasema: (Luut'i) Hakika hawa wageni wangu, basi msinifedheheshe.68

    Maelezo
    [68] Luut'i akaogopa wasije wakatenda vitendo vyao viovu. Akasema: Hawa ni wageni wangu, basi msinifedheheshe kwa vitendo vyenu vibaya.
  69. وَٱتَّقُوا۟ ٱللَّهَ وَلَا تُخْزُونِ۝٦٩

    Waittaqoo Allaha wala tukhzooni

    Na mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi.69

    Maelezo
    [69] Na mwogopeni Mwenyezi Mungu Mtukufu! Msifanye uchafu wenu, mkanipatisha hizaya na madhila mbele yao!
  70. قَالُوٓا۟ أَوَلَمْ نَنْهَكَ عَنِ ٱلْعَـٰلَمِينَ۝٧٠

    Qaloo awalam nanhaka ʿani alʿalameena

    Wakasema: Sisi hatukukukataza usimkaribishe yeyote?70

    Maelezo
    [70] Wale wakhalifu wakasema: Kwani si tulikukataza wewe usimkaribishe mtu yeyote, na hivi sasa tena unatuzuia tusifanye nao tunayo yatamani?
  71. قَالَ هَـٰٓؤُلَآءِ بَنَاتِىٓ إِن كُنتُمْ فَـٰعِلِينَ۝٧١

    Qala haolai banatee in kuntum faʿileena

    Akasema: Hawa binti zangu, ikiwa nyinyi ni watendaji.71

    Maelezo
    [71] Ili kuwanabihisha njia ya maumbile ya kisharia, Nabii wa Mwenyezi Mungu Luut'i akasema: Hawa mabinti wa mji huu, nao ni binti zangu, waoeni ikiwa mnataka kukidhi matamanio yenu.
  72. لَعَمْرُكَ إِنَّهُمْ لَفِى سَكْرَتِهِمْ يَعْمَهُونَ۝٧٢

    Laʿamruka innahum lafee sakratihim yaʿmahoona

    Naapa kwa umri wako! Hakika hao walikuwa katika ulevi wao, wakihangaika ovyo.72

    Maelezo
    [72] Ewe Nabii Muaminifu! Naapa kwa haki ya uhai wako! Hawa wamo katika mghafala, hawajui yatakayo wateremkia. Wamekuwa kama walio lewa! Hakika wao wamo katika upotovu, wanatapatapa, hawajui wapite wapi.
  73. فَأَخَذَتْهُمُ ٱلصَّيْحَةُ مُشْرِقِينَ۝٧٣

    Faakhathathumu alssayhatu mushriqeena

    Ukelele ukawatwaa wakipambaukiwa.73

    Maelezo
    [73] Na walipo kuwa wao wamo katika ulevi wao wa mghafala nyoyo zao na akili zao zikachotwa na ukelele mkali mno wa kutisha, wakati jua lilipo chomoza.
  74. فَجَعَلْنَا عَـٰلِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهِمْ حِجَارَةً مِّن سِجِّيلٍ۝٧٤

    Fajaʿalna ʿaliyaha safilaha waamtarna ʿalayhim hijaratan min sijjeelin

    Na tukaigeuza nchi juu chini, na tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo wa Motoni.74

    Maelezo
    [74] Mwenyezi Mungu Aliye takasika katekeleza hukumu yake, akasema: Miji yao tukaifanya juu chini kwa kuivuruga, na tukawateremshia udongo ulio fanyika mawe ukiwateremkia kama mvua. Majumba yao yakaporomoka. Na wakitoka nje hukuta hiyo mvua ya mawe. Kwa hivyo wakawa wamezungukwa kila jiha. (upande)
  75. إِنَّ فِى ذَٰلِكَ لَـَٔايَـٰتٍ لِّلْمُتَوَسِّمِينَ۝٧٥

    Inna fee thalika laayatin lilmutawassimeena

    Hakika katika hayo zipo ishara kwa waaguzi.75

    Maelezo
    [75] Haya yaliyo washukia kaumu Luut'i ni alama wazi ya kuonyesha vipi Mwenyezi Mungu Mtukufu anavyo timiza ahadi yake. Wajuao mambo wanayatambua hayo, na wanayaelewa matokeo yake kwa alama zake, kwani kila kitendo chenye sifa ya ukosefu kina alama yake isiyo potea. Matokeo yake ni mfano wa haya, duniani na Akhera.
  76. وَإِنَّهَا لَبِسَبِيلٍ مُّقِيمٍ۝٧٦

    Wainnaha labisabeelin muqeemin

    Na miji hii ipo kwenye njia inayo pitiwa.76

    Maelezo
    [76] Na mabaki ya mji huu yapo yamesalia. Nayo yapo njiani katika njia inayo pitiwa na watu. Anaye taka kuwaidhika kwayo anaweza kuwaidhika.
  77. إِنَّ فِى ذَٰلِكَ لَـَٔايَةً لِّلْمُؤْمِنِينَ۝٧٧

    Inna fee thalika laayatan lilmumineena

    Hakika katika hayo ipo ishara kwa Waumini.77

    Maelezo
    [77] Kwa kuwa mabaki yake yapo kwenye njia iliyo wazi ni dalili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kutimiza onyo lake, na Waumini wenye kut'ii Haki wanatambua hayo.
  78. وَإِن كَانَ أَصْحَـٰبُ ٱلْأَيْكَةِ لَظَـٰلِمِينَ۝٧٨

    Wain kana ashabu alaykati lathalimeena

    Na Hakika watu wa kichakani, walikuwa wenye kudhulumu78

    Maelezo
    [78] Kama kaumu ya Luut'i walivyo kadhibisha, kadhaalika wakaazi wa Kichakani kwenye msitu wenye matunda walimkanya Mtume wao. Wakawa madhaalimu wenye kudhulumu mno katika imani yao na maingiliano yao.
  79. فَٱنتَقَمْنَا مِنْهُمْ وَإِنَّهُمَا لَبِإِمَامٍ مُّبِينٍ۝٧٩

    Faintaqamna minhum wainnahuma labiimamin mubeenin

    Kwa hivyo tukawaadhibu. Na nchi mbili hizi ziko kwenye njia iliowazi.79

    Maelezo
    [79] Tukawateremshia nakama yetu. Na mabaki yao yapo njiani yanaonekana, na mpita njia akiwa ni mtu wa Imani basi anaweza kuzingatia kwayo.
  80. وَلَقَدْ كَذَّبَ أَصْحَـٰبُ ٱلْحِجْرِ ٱلْمُرْسَلِينَ۝٨٠

    Walaqad kaththaba ashabu alhijri almursaleena

    Na bila ya shaka wakaazi wa Hijr waliwakanusha Mitume.80

    Maelezo
    [80] Na kama walio tangulia hali kadhaalika wakaazi wa Hijr walimkanusha Mtume wao aliye tumwa kwao, na kwa hivyo wakawa wamewakanusha Mitume wote. Kwani ujumbe wa Mwenyezi Mungu ni mmoja. Watu wa Hijr ndio Thamud. Na Hijr ni bonde baina ya Madina na Sham. Tazama maelezo juu ya Aya 73 ya Surat Al-Aa'raaf.
  81. وَءَاتَيْنَـٰهُمْ ءَايَـٰتِنَا فَكَانُوا۟ عَنْهَا مُعْرِضِينَ۝٨١

    Waataynahum ayatina fakanoo ʿanha muʿrideena

    Na tuliwapa ishara zetu, nao wakazipuuza.81

    Maelezo
    [81] Tuliwabainishia hoja zenye kuonyesha uwezo wetu, na Utume wa Mtume wetu, nao wakayapuuza, wala wasiyafikiri.
  82. وَكَانُوا۟ يَنْحِتُونَ مِنَ ٱلْجِبَالِ بُيُوتًا ءَامِنِينَ۝٨٢

    Wakanoo yanhitoona mina aljibali buyootan amineena

    Nao walikuwa wakichonga majumba katika milima kwa amani.82

    Maelezo
    [82] Nao walikuwa watu wenye nguvu na wajenzi. Walikuwa wakijenga majumba yao katika milima na wakiichonga hiyo hiyo milima. Na wao walikuwa wakijiamini kuwa wametua na nafsi zao na mali yao.
  83. فَأَخَذَتْهُمُ ٱلصَّيْحَةُ مُصْبِحِينَ۝٨٣

    Faakhathathumu alssayhatu musbiheena

    Basi ukelele ukawatwaa asubuhi.83

    Maelezo
    [83] Walipo kufuru na wakakanya, zikawajia sauti za kutisha, za kuonya kuteketea kwao, wakahiliki wakati wa asubuhi.
  84. فَمَآ أَغْنَىٰ عَنْهُم مَّا كَانُوا۟ يَكْسِبُونَ۝٨٤

    Fama aghna ʿanhum ma kanoo yaksiboona

    Hayakuwafaa waliyo kuwa wakiyachuma.84

    Maelezo
    [84] Wala mali waliyo yachuma na majumba waliyo yajenga hayakuwalinda na hilaki iliyo wateremkia.
  85. وَمَا خَلَقْنَا ٱلسَّمَـٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَآ إِلَّا بِٱلْحَقِّ ۗ وَإِنَّ ٱلسَّاعَةَ لَـَٔاتِيَةٌ ۖ فَٱصْفَحِ ٱلصَّفْحَ ٱلْجَمِيلَ۝٨٥

    Wama khalaqna alssamawati waalarda wama baynahuma illa bialhaqqi wainna alssaʿata laatiyatun faisfahi alssafha aljameela

    Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ila kwa ajili ya Haki. Na hakika Kiyama kitafika. Basi samehe msamaha mzuri.85

    Maelezo
    [85] Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo kati yao katika anga, na viliomo ndani yake, watu na wanyama, na mimea na visio na uhai, na vinginevyo ambavyo mwanaadamu havijui, isipo kuwa kwa uadilifu, na hikima, na maslaha ambayo hayaambatani na fisadi ya kudumu isiyo na mwisho. Na kwa hivyo basi ni lazima siku ya kukomesha shari ifike bila ya shaka yoyote. Basi ewe Nabii Mtukufu! Wasamehe hao washirikina adhabu ya duniani, na ingiana nao kwa kuwastahamilia maudhi yao. Na kuwaita wito kwa hikima ni kuingiliana kwa usamehevu na upole.
  86. إِنَّ رَبَّكَ هُوَ ٱلْخَلَّـٰقُ ٱلْعَلِيمُ۝٨٦

    Inna rabbaka huwa alkhallaqu alʿaleemu

    Hakika Mola wako Mlezi ndiye Muumbaji Mjuzi.86

    Maelezo
    [86] Ewe Nabii! Mwenyezi Mungu aliye kuumba na akakulea, ni Mwenye viumbe vyote, na anajua hali yako na yao. Yeye anastahiki umtegemezee mambo yako na yao. Naye anajua maslaha yako na yao.
  87. وَلَقَدْ ءَاتَيْنَـٰكَ سَبْعًا مِّنَ ٱلْمَثَانِى وَٱلْقُرْءَانَ ٱلْعَظِيمَ۝٨٧

    Walaqad ataynaka sabʿan mina almathanee waalqurana alʿatheema

    Na tumekupa Aya saba zinazo somwa mara kwa mara, na Qur'ani Tukufu.87

    Maelezo
    [87] Ewe Nabii Muaminifu, tumekupa Aya saba za Qur'ani, nazo ni Sura ya Al- Fatiha unayo ikariri katika kila Swala, na humo yamo ya kutunyenyekea na maombi ya uwongofu yaliyo kaamili. Na tumekupa Qur'ani Tukufu yote. Na ndani yake mna hoja, na miujiza. Kwa hivyo wewe una nguvu ambazo zinakufalia usamehe.
  88. لَا تَمُدَّنَّ عَيْنَيْكَ إِلَىٰ مَا مَتَّعْنَا بِهِۦٓ أَزْوَٰجًا مِّنْهُمْ وَلَا تَحْزَنْ عَلَيْهِمْ وَٱخْفِضْ جَنَاحَكَ لِلْمُؤْمِنِينَ۝٨٨

    La tamuddanna ʿaynayka ila ma mattaʿna bihi azwajan minhum wala tahzan ʿalayhim waikhfid janahaka lilmumineena

    Usivitumbulie macho yako vitu tulivyo waneemesha makundi fulani kati yao, wala usiwahuzunikie. Na wainamishie bawa lako (la huruma) Waumini.88

    Maelezo
    [88] Ewe Mtume! Usivitazame kwa kuvitamani na kuvitaka vitu vya starehe ya dunia tulivyo wapa makafiri wa kishirikina, na Kiyahudi, na Kikristo, na Kimajusi. Kwani hivyo ni duni kwa kulinganisha na ulio pewa wewe katika kuwasiliana nasi, na Qur'ani Tukufu. Wala usiwasikitikie kwa sababu ya kuendelea kwao na madhambi. Nawe tulia, na unyenyekee, na wachukue Waumini ulio nao kwa upole. Kwani hao ni nguvu za Haki, na watu wa Mwenyezi Mungu.
  89. وَقُلْ إِنِّىٓ أَنَا ٱلنَّذِيرُ ٱلْمُبِينُ۝٨٩

    Waqul innee ana alnnatheeru almubeenu

    Na sema: Hakika mimi ni mwonyaji mwenye kubainisha.89

    Maelezo
    [89] Ewe Nabii! Waambie makafiri wote: Mimi nakuonyeni na adhabu kali, na nakubainishieni maonyo yangu kwa hoja za kukata.
  90. كَمَآ أَنزَلْنَا عَلَى ٱلْمُقْتَسِمِينَ۝٩٠

    Kama anzalna ʿala almuqtasimeena

    Kama hivyo tuliwateremshia walio gawa,90

    Maelezo
    [90] Haya ni kama maonyo ya walio igawanya Qur'ani wakaifanya ati ni mashairi, na ukohani, na hadithi za kale na mengineyo. Nao wasiiamini juu ya kusimama hoja juu yao.
  91. ٱلَّذِينَ جَعَلُوا۟ ٱلْقُرْءَانَ عِضِينَ۝٩١

    Allatheena jaʿaloo alqurana ʿideena

    Ambao wakaifanya Qur'ani vipande vipande.91

    Maelezo
    [91] Hao waliifanya Qur'ani vipande mbali mbali, nayo hali kuwa haikubali kugawika kwa umuujiza wake na ukweli wake.
  92. فَوَرَبِّكَ لَنَسْـَٔلَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ۝٩٢

    Fawarabbika lanasalannahum ajmaʿeena

    Basi Naapa kwa Mola wako Mlezi! Tutawahoji wote.92

    Maelezo
    [92] Ikiwa hiyo hali yao, basi Wallahi kwa Aliye kuumba akakulinda na akakulea, hapana shaka tutawahisabu wote Siku ya Kiyama,
  93. عَمَّا كَانُوا۟ يَعْمَلُونَ۝٩٣

    ʿAmma kanoo yaʿmaloona

    Kwa waliyo kuwa wakiyatenda.93

    Maelezo
    [93] Kwa vitendo vyao vya kuudhi, na kufuru, na kejeli.
  94. فَٱصْدَعْ بِمَا تُؤْمَرُ وَأَعْرِضْ عَنِ ٱلْمُشْرِكِينَ۝٩٤

    Faisdaʿ bima tumaru waaʿrid ʿani almushrikeena

    Basi wewe yatangaze uliyo amrishwa, na jitenge na washirikina.94

    Maelezo
    [94] Basi wewe tangaza wito wa Haki, wala usishughulike na wayatendao washirikina na maneno yao.
  95. إِنَّا كَفَيْنَـٰكَ ٱلْمُسْتَهْزِءِينَ۝٩٥

    Inna kafaynaka almustahzieena

    Hakika Sisi tunatosha kukukinga na wanao kejeli.95

    Maelezo
    [95] Na hao washirikina wanao ukejeli wito wako hawatokushinda, wala hawatoweza kukuingilia kati baina yako na wito wako.
  96. ٱلَّذِينَ يَجْعَلُونَ مَعَ ٱللَّهِ إِلَـٰهًا ءَاخَرَ ۚ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ۝٩٦

    Allatheena yajʿaloona maʿa Allahi ilahan akhara fasawfa yaʿlamoona

    Hao wanao fanya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu yupo mungu mwingine.Basi, watakuja jua!96

    Maelezo
    [96] Hao washirikina mawazo yao yamedhoofika, ndio wakafanya kuwa Mwenyezi Mungu anao miungu mingine ya masanamu. Na watakuja jua matokeo ya ushirikina wao itapo wateremkia adhabu chungu.
  97. وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدْرُكَ بِمَا يَقُولُونَ۝٩٧

    Walaqad naʿlamu annaka yadeequ sadruka bima yaqooloona

    Na Sisi tunajua kwa hakika kuwa wewe kifua chako kinaona dhiki kwa hayo wayasemayo.97

    Maelezo
    [97] Nasi tunajua dhiki ya moyo inayo kupata kwa wanayo yasema ya ushirikina na kejeli na dharau.
  98. فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَكُن مِّنَ ٱلسَّـٰجِدِينَ۝٩٨

    Fasabbih bihamdi rabbika wakun mina alssajideena

    Basi mtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi, na uwe miongoni wanaomsujudia.98

    Maelezo
    [98] Ikikupata dhiki hiyo mkimbilie Mwenyezi Mungu Mtukufu umwelekee, na umt'ii na umnyenyekee, na utake msaada kwa Sala, kwani humo ndio imo poza.
  99. وَٱعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ ٱلْيَقِينُ۝٩٩

    Waoʿbud rabbaka hatta yatiyaka alyaqeenu

    Na muabudu Mola wako Mlezi mpaka ikufikie Yakini. (nao ni Mauti)99

    Maelezo
    [99] Na shikilia ibada ya Mwenyezi Mungu aliye kuumba, akakulinda, mpaka ifike amri ya yakini, nayo ni Mauti.

Maswali yanayoulizwa mara kwa mara

Surat Al-Hijr maana yake ni nini?

Al-Hijr maana yake ni “Eneo la Miamba”.

Surat Al-Hijr iko katika juzuu ya ngapi?

Surat Al-Hijr iko katika juzuu ya 14.

Surat Al-Hijr ina aya ngapi?

Surat Al-Hijr ina aya 99.

Surat Al-Hijr ni ya Makka au ya Madina?

Surat Al-Hijr ni sura ya Makka.

Surat Al-Hijr ni sura ya ngapi katika Qur’ani?

Ni sura ya 15 katika Qur’ani.

Vyanzo

  • Arabic text: Tanzil Quran Text (Uthmani) (Tanzil Project, CC BY 3.0), reproduced without changes.
  • Translation: Ali Muhsin Al-Barwani, from QuranEnc.com, version 1.0.1, reproduced without changes.
  • Transliteration: Tanzil.net English transliteration.
  • Recitation: Mishary Rashid Alafasy, via QuranicAudio.com and EveryAyah.com.
  • Word by word: recordings and meanings from Quran.com (Quran Foundation), played when you tap a word.
  • Madinah and IndoPak fonts (Settings): the text in those scripts and their fonts come from the Quran Foundation (Quran.com); the Madinah font is the King Fahd Glorious Quran Printing Complex's Uthmanic Hafs font.

Found a mistake? Report a mistake and we will check it against the source.

Mipangilio ya kusoma

Fonti ya Qur’ani
Ukubwa wa Kiarabu
100%
Ukubwa wa tafsiri
100%
Mandhari

Ongeza kwenye skrini ya kwanza

ReadSurahFungua ReadSurah kutoka skrini ya kwanza, kwa skrini nzima. Sura ulizosoma hufunguka hata bila intaneti.

  1. Katika Safari, gusa kitufe cha kushiriki (Share). Kwenye iPhone mpya kiko kwenye menyu ya •••.
  2. Gusa “Add to Home Screen”. Huenda ukahitaji kusogeza chini.
  3. Gusa “Add”.